Moshi.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC, imezindua maadhimisho ya Siku ya Usikivu Duniani kwa mwaka 2025 kwa kutoa huduma za milango ya fahamu, ikiwemo huduma za sikio, pua, na koo bure kwa wananchi lengo likiwa ni kurudisha huduma kwa jamii.
Kilele cha Maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Jumatatu, Machi 3, 2025, ambapo huduma za bure zitapatikana kwa siku tatu mfululizo kuanzia Machi 1, 2025.
Huduma hii ni fursa muhimu kwa wananchi, hasa kwa wale ambao hawana uwezo wa kupata huduma hizo katika hospitali za binafsi ambapo KCMC imejizatiti kutoa huduma bora na za kisasa ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata matibabu bora kwa bei nafuu au bure.
Akizungumza na vyombo vya habari, Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, Gabriel Chiseo, alisema kuwa ni muhimu kwa hospitali hiyo kusaidia jamii kwa kutoa huduma hizo bure ili kupunguza mzigo wa matatizo ya milango ya fahamu ambayo mara nyingi huwa ni changamoto kwa wananchi wengi, hasa katika maeneo ya vijijini.
KCMC imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma bora za afya kwa wakazi wa Kaskazini na maeneo mengine, na imejizatiti kuwa ni chombo cha kusaidia jamii hasa kwa kipindi hiki cha changamoto za kiafya zinazohitaji usikivu na huduma za haraka. Huduma hizi za bure ni sehemu ya juhudi za hospitali hiyo kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na huduma za afya.
Mwisho.
0 Comments